Back

ⓘ Mapigano ya Marathoni
Mapigano ya Marathoni
                                     

ⓘ Mapigano ya Marathoni

Mapigano ya Marathoni yalifanyika mnamo Septemba 490 KK kwenye uwanda wa Marathoni, si mbali na Athens, Ugiriki. Yalipigwa kati ya jeshi la Athens na Waajemi. Athens iliungwa mkono na kikosi kidogo kutoka mji wa Plataia. Ushindi wa Athens ulimaliza jaribio la kwanza la Uajemi ya Kale kupata kipaumbele katika Ugiriki.

Uvamizi wa Uajemi ulikuwa jibu la ushiriki wa Athens katika uasi wa Ionia. Hapo miji ya Athens na Eretria iliwahi kutuma kikosi kusaidia miji ya Ionia, ambayo ilikuwa ikijaribu kupindua utawala wa Uajemi. Waathens na Eretria walifanikiwa kukamata na kuchoma Sardis makao makuu ya gavana wa Uajemi, lakini walilazimika kurudi nyuma na hasara kubwa. Kwa kujibu uvamizi huu, mfalme Dario I wa Uajemi aliapa kuchoma Athens na Eretria.

                                     

1. Uvamizi wa Waajemi

Mara tu uasi wa Ionia ulipoangamizwa na Waajemi, mfalme Dario alianza kupanga adhabu ya miji ya Kigiriki waliompinga. Mnamo 490 KK alituma kikosi chini ya majenerali Datis na Artaphernes waliovuka Bahari ya Aegean, ili kuteka Visiwa vya Kikladi katika bahari hiyo. Hatua iliyofuata ilikuwa kushambulia mji wa Eretria. Waajemi wakakamata na kuchoma Eretria.

Kutoka hapo Waajemi walipanda meli zao kwenda Attika, rasi kubwa ya Ugiriki ambako Athens iko. Walifika kwenye hori ya Marathoni.

                                     

2. Mapigano

Marathoni pana uwanja mpana uliofaa kwa jeshi lao maana ilikuwa na tambarare ambako jeshi la farasi lilipewa nafasi nzuri. Waathens, waliojiunga na kikosi kidogo kutoka mji wa Plataia, walikimbia kwenda Marathoni walipofaulu kuzuia njia kutoka katika tambarare ya Marathoni. Majeshi yalitazamana kwa siku tano hivi.

Hali halisi si rahisi kuelewa kutokana na taarifa zilizohifadhiwa ambazo zote ziliandikwa kitambo baadaye. Hatimaye Wagiriki walishambulia Waajemi. Inawezekana shambulio hilo lilitokea wakati farasi wa Waajemi walihamishwa tena kwenye meli kwa sababu jemadari Mwajemi aliamua kuhama. Kwa namna yoyote, jeshi la farasi upande wa Waajemi halikushiriki katika mapigano na askari wa Athens wenye nguo za kinga walishinda wanajeshi wa miguu wa Waajemi waliokuwa na silaha nyepesi zaidi. Walipiga mabawa ya Uajemi kabla ya kugeukia katikati ya mstari wa Uaji. Waathens walikamata manowari saba lakini manowari nyingine ziliweza kukimbia. Athens ilipoteza raia 192 lakini haijulikani walipoteza watumwa na watu wengine wasiokuwa raia huru. Waajemi walisemekana kupoteza watu 6000.

                                     

3. Matokeo

Ushindi wa Marathoni ulikuwa mwisho wa jaribio la kwanza la Uajemi kuvamia Ugiriki. Jeshi la Kiajemi lilirudi upande wa Asia Ndogo. Mfalme Dareio alikuwa na hasira akaanza kuandaa jeshi kubwa kwa kulipiza kisasi, lakini mnamo mwaka 486 KK uasi huko Misri -sehemu ya Dola la Uajemi- ulimlazimisha kuachana na mipango hiyo. Baada ya kifo cha Dario, mwana na mwandamizi wake Xerxes I aliandaa uvamizi mwingine wa Ugiriki ulioanza mnamo 480 KK.

                                     

4. Asili ya Mbio za Marathon

Kufuatana na hadithi inayosimuliwa mahali pengi, kijana alikimbia kutoka Marathoni hadi Athens kuleta habari za ushindi. Hadithi hiyo ni chanzo cha Mbio ya Marathoni ambao ni mbio ya urefu mkubwa wa km 42.195 katika riadha ya kimataifa na sehemu ya mashindano wakati wa Michezo ya Olimpiki ya kisasa.

Masimulizi hayo si ya kihistoria; msingi wake ni taarifa ya Herodoti aliyeandika kwamba kijana alitumwa kutoka Athens kwenda Sparta kuomba msaada dhidi ya uvamizi wa Uajemi; kijana huyu alipita kilomita 225 hadi Sparta akafika siku iliyofuata. Halafu katika kisa tofauti, Herodoti aliandika kwamba jeshi la Athens baada ya mapigano lilirudi kwa kasi kubwa iwezekanavyo kilomita 40 kutoka Marathon hadi Athens kwa sababu walihofia Waajemi wangejaribu kuvamia mji kwa njia ya meli zao; walipofika jioni waliona jahazi za Waajemi zikikaribia. Lakini Waajemi walipotambua jeshi la Athens lilikuwa limerudi na kuwa tayari, walirudi kwao.

Baadaye, lakini tayari nyakati za Roma ya Kale, masimulizi hayo yaliunganishwa kuwa moja ambako kijana aliyepewa mara nyingi jina la Philippides alikimbilia Athens kupeleka habari za ushindi; katika simulizi hilo aliweza kutamka "Tumeshinda" kabla ya kuanguka chini na kufa kwa uchovu. Wakati michezo ya Olimpiki ilipoanzishwa upya katika karne ya 19, hadithi hiyo ilifufuliwa na kuwa msingi kwa mashindano ambako wakimbiaji wanashindana kwa urefu wa kilomita 41.195 kwenye mbio za Marathon.                                     
  • hii inahusu mwaka 490 KK. Mapigano ya Marathoni nchini ya Ugiriki jeshi la Wagiriki linashinda uvamizi wa Waajemi chini ya mfalme Dareio I Wikimedia
  • Mbio ya Marathoni ni mbio ya masafa marefu kuliko zote, ikichukua kilometa 42.195. Ndiyo kilele cha michezo ya Olimpiki. Asili ya mchezo huo ni mbio ya urefu

Users also searched:

...
...
...