Back

ⓘ Anofelesi
Anofelesi
                                     

ⓘ Anofelesi

Anofelesi ni spishi za mbu za jenasi Anopheles katika familia Culicidae. Zaidi ya spishi 100 zinaweza kueneza malaria ya watu, lakini spishi 30-40 tu ni muhimu sana. Katika Afrika anofelesi wa Gambia ni muhimu kabisa, kwa sababu anatokea mahali pengi kusini kwa Sahara na hueneza spishi ya malaria hatari sana, Plasmodium falciparum. Hapo majuzi spishi nyingine, anofelesi wa Asia, amefika Pembe ya Afrika. Spishi hiyo ni hatari kwa sababu inaweza kuishi mijini kwa urahisi kuliko anofelesi wa Gambia, kwa hiyo inaweza kuongeza visa vya malaria katika Afrika.

                                     

1. Maelezo

Kama mbu wote, wapevu wa anofelesi wana mwili mwembamba wenye sehemu tatu: kichwa, toraksi na fumbatio.

Kichwa kimetoholewa kwa kupata taarifa ya hisia na kwa kujilisha. Kina macho na jozi ya vipapasio virefu vyenye pingili nyingi. Vipapasio ni muhimu kwa kugundua harufu ya kidusiwa na pia harufu ya maeneo ya kuzaliana ambapo majike hutaga mayai. Sehemu za kinywa zinaunda mrija mrefu unaoelekea mbele na unaotumika kujilisha. Maksila zinabeba palpi zilizo na vipokezi vya dioksidi kabonia, kivutio kikubwa kinachoonyesha yupo wapi kidusiwa wa mbu.

Toraksi imetoholewa kwa mwendo. Jozi tatu za miguu na jozi moja ya mabawa zimeunganishwa kwenye toraksi.

Fumbatio limetoholewa kwa kumengenya chakula na kuzalisha mayai. Sehemu hii yenye pingili huvimba sana wakati jike anapofyonza damu ambayo ni chanzo cha protini kwa uzalishaji wa mayai.

Anofelesi wanaweza kutofautishwa na mbu wengine kwa palpi zilizo ndefu kama mrija na kwa uwepo wa mabaka ya vigamba vyeusi na vyeupe juu ya mabawa. Wapevu wanaweza pia kutambuliwa kwa mkao wao wa kawaida wa kupumzika: wakikaa mahali huweka fumbatio lao kwa pembe badala ya sambamba na uso ambapo wanapumzika tazama mchoro.

Madume na majike wote hula mbochi na vitu vingine vyenye sukari, lakini majike wanahitaji mlo wa damu kwa kila kundi la mayai ambalo hukua katika ovari zake. Spishi nyingi zinaweza kuchukua damu kutoka kwa wanyama wengi, haswa mamalia, lakini nyingine huchagua spishi chache na kadhaa hupendelea watu.

Majike hutaga makundi ya mayai 50-200 kila siku 2-3. Kwa kuzingatia kuwa wastani wa maisha ni kama wiki mbili, makundi 5-6 hutagwa na kila jike, ingawa hii inaweza kuwa chache zaidi ikiwa jike atashindwa kupata mlo wa damu kwa wakati. Mayai ni madogo kiasi karibu mm 0.5 x 0.2. Mayai hutagwa peke yao na moja kwa moja juu ya maji. Hayo ni wa kipekee kwa kuwa yana kibunzi kila upande. Hutoa lava ndani ya siku 2-3 katika ukanda wa tropiki lakini hii inaweza kuchukua hadi wiki 2-3 katika maji baridi. Mayai siyo sugu kwa kukausha.

Lava au mabuu ya anofelesi wana kichwa kilichokua vizuri chenye brashi za kinywa zinazotumiwa kujilisha, toraksi kubwa na fumbatio lenye pingili tisa. Hawana miguu. Kinyume na mbu wengine hawana neli ya kupumua, kwa hivyo hujiweka ili mwili wao uwe sambamba na uso wa maji. Walakini, ili kupumua mabuu ya spishi zisizo anofelesi hujiambatisha na uso wa maji kwa neli yao ya nyuma, na mwili wao ukielekea chini angalia mchoro.

Mabuu hupumua kupitia spirakulo zilizopo kwenye pingili ya nane ya fumbatio, kwa hivyo lazima waje kwenye uso mara kwa mara. Wanatumia wakati wao mwingi kujilisha na miani, bakteria, na vijidudu vingine kwenye tabaka jembamba la uso. Huzama chini ya uso tu wakati wanasumbuliwa. Mabuu huogelea ama kwa mashtuko ya mwili mzima au kwa kusukuma kwa brashi ya kinywa.

Mabuu hukua kupitia hatua nne, kisha hubadilika kuwa mabundo. Mwishoni kwa kila hatua mabuu huambua kiunzi-nje, au ngozi, kuwezesha ukuaji zaidi. Mabuu ya hatua ya kwanza wana urefu wa karibu mm 1, huku mabuu ya hatua ya nne kwa kawaida wawe na urefu wa mm 5-8.

Mabuu hutokea katika makazi anuwai, lakini spishi nyingi hupendelea maji safi yasiyonajisiwa. Mabuu ya anofelesi wamepatikana katika maji baridi au vinamasi vya maji ya chumvi, kapa, mashamba ya mpunga, mitaro yenye nyasi, kingo za vijito na mito na mabwawa madogo ya mvua ya muda mfupi. Spishi nyingi hupendelea makazi yenye mimea. Wengine wanapendelea makazi bila mimea. Fulani huzaa katika mabwawa ya wazi yenye mwanga wa jua huku wengine wapatikane tu kwenye maeneo ya kuzaliana kwa kivuli kwenye misitu. Spishi chache huzaa kwenye mashimo ya miti au makwapajani ya mimea fulani. Mwishowe, spishi nyingine huzaa katika vitu vilivyojazwa maji na vilivyotengenezwa na bidamu kama madebe, vyombo vya plastiki, matangi ya maji na hata tairi zilizotupwa.

Mabundo wana umbo la mkato wakitazamwa kutoka upande. Kichwa na toraksi zimeunganishwa kwenye kefalotoraksi na fumbatio limezunguka chini. Kama mabuu, sharti mabundo waje kwenye uso wa maji mara kwa mara ili kupumua, ambayo hufanya kupitia jozi ya tarumbeta za kupumua kwenye kefalotoraksi yao. Baada ya siku chache kama bundo, ngozi ya juu ya kefalotoraksi inapasuka na mbu mpevu huibuka. Hatua ya bundo hudumu siku 1-3 kulingana na nyuzijoto ya maji.

                                     

2. Spishi kadhaa za Afrika

  • Anopheles funestus, Anofelesi Kamata
  • Anopheles arabiensis, Anofelesi Arabu
  • Anopheles nili, Anofelesi wa Kameruni
  • Anopheles gambiae, Anofelesi wa Gambia
  • Anopheles stephensi, Anofelesi wa Asia

Users also searched:

...
...
...